KOCHA WA AZAM FC ASEMA TATIZO LA UFUNGAJI LINAANZA KUMALIZIKA




KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, amesema kuwa tatizo la ufungaji kwa timu yake linaelekea kumalizika kutokana na safu yake ya ushambuliaji kuonyesha kiwango kizuri kwenye ushindi wa mabao 3-0 walioupata dhidi ya Majimaji ya Songea jana jioni.
Kocha huyo amekuwa akielezea mara kwa mara tatizo hilo kwenye kikosi chake kufuatia wachezaji wake kupoteza nafasi nyingi za wazi kwenye mechi zilizopita kabla ya kuivaa Majimaji.
Mabao ya Azam FC inayoongoza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ikiwa na pointi nne sawa na Simba, Tanzania Prisons na Ruvu Shooting, yaliwekwa kimiani na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga mawili na Mudathir Yahya akitupia jingine.
Mabao hayo mawili yamemfanya Bocco kufikisha jumla ya mabao matatu kwenye mechi mbili za ligi msimu huu na kuwa kinara wa ufungaji mabao ndani ya michuano hiyo, jingine akifunga Azam FC ilipotoa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza dhidi ya African Lyon.
Zeben aliuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo, kuwa tatizo hilo linaanza kuondoka baada ya kuwapa mbinu kadhaa wachezaji wake pamoja na kujifunza kupitia mechi zilizopita.  
“Mechi ya leo (jana) tumeshinda baada ya wachezaji kupoea vema maelekezo tuliyokuwa tukiwapa, hata hivyo tulipoingia kipindi cha kwanza wachezaji walikuwa na wasiwasi lakini kipindi cha pili tuliwaambia watulie na kweli wakafuta kile tulichowaambia na kupata tulichopata, na ndio maana mechi hiyo haikuonekana ngumu sana kama nyingine zilizopita,” alisema.
Alisema: “Mwanzo tulikuwa tunashindwa kutumia nafasi tunazopata lakini mazoezi niliyokuwa nawapa wachezaji wangu kwa kipindi cha wiki hii yote yamewasaidia, nilikuwa najaribu kuwapa maelekezo kuwa wakifika kwenye eneo la mwisho la kumalizia cha msingi kinachotakiwa ni mabao.”
Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, alisema kuwa mbali na kuanza kulitatua tatizo hilo, pia amedai kikosi chake kimeanza kuimarika kuliko kilivyokuwa awali jambo ambalo limewafanya kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo na kufunga mabao zaidi.
Kuelekea mechi za Mbeya
Akizungumzia mechi mbili zijazo za ugenini zitakazofanyika mkoani Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons (Septemba 7) na Mbeya City (Septemba 10), alisema amejipanga kuwapa mbinu tofauti wachezaji wake ili kuweka kukabiliana na mazingira ya huko pamoja na Uwanja wa Sokoine.
“Baada ya ushindi wa leo, kesho (Jumapili) wachezaji wangu watapumzika na kuanza mazoezi Jumatatu (kesho) hapo ndipo tutaanza kujadili namna ya kucheza mechi hizo za nje ya Chamazi, kwani sehemu tutakayochezea itakuwa ni tofauti na hapa Chamazi, kwa hiyo tutakuwa tukipeana mbinu na njia za kuendana na uwanja tutakaokuwa tukichezea,” alimazia Zeben.


No comments