AZAM FC WABEBA MAKOMBORA KUIFUATA MBEYA CITY
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuelekea mkoani Mbeya kesho Ijumaa alfajiri ikiwa imejidhatiti kuzoa pointi zote tatu itakapoivaa Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Sokoine, jijini Jumapili hii.
Azam FC inaelekea mkoani humo ikiwa na kumbukumbu ya kutolewa na Mtibwa Sugar kwenye Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) wikiendi iliyopita kwa mikwaju ya penalti 9-8 kufuatia dakika 90 kumalizika kwa suluhu.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Jaffar Idd, ameweka wazi jana kuwa wanaenda huko kupambana kwa lengo la kuibuka na ushindi ili kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.
“Tunakwenda kupambana kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunacheza na kupata pointi tatu muhimu ili tuzidi kuimarika katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini timu ya Azam inatarajia kuondoka hapa Dar es Salaam siku ya Ijumaa (kesho) tayari kwa safari ya kuelekea Mbeya tayari kwa mchezo huo (vs Mbeya City) katika Uwanja wa Sokoine ambao utachezwa Jumapili,” alisema.
Timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza iliyofanyika Uwanja wa Azam Complex, Azam FC ilishinda bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Mbaraka Yusuph, ambaye tayari jana Jumatano ameanza mazoezi na wenzake baada ya majeraha ya nyama za paja kupona.
Azam FC itaelekea huko bila mabeki wake, Daniel Amoah, David Mwantika ambao ni wagonjwa huku Bruce Kangwa, akikosekana kutokana na kutumikia adhabu ya kukosa mechi moja baada ya kukusanya kadi tatu za njano, pia Wazir Junior, aliyepumzishwa kwa siku tano, akitarajia kuanza rasmi mazoezi mepesi ya mchangani leo Alhamisi.
Hadi sasa kwenye msimamo wa ligi hiyo, Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 44 ikizidiwa pointi mbili na Yanga iliyo nafasi ya pili kwa pointi 46 huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 49, timu hizo mbili za juu zikiwa na mchezo mmoja mkononi kila mmoja.
Post a Comment