AZAM FC YASHIKANI USUKANI WA LIGI YA VODACOM.
Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanikiwa kushika usukani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Kagera Sugar bao 1-0 katika mechi iliyopigwa hapo jana kwenye uwanja wao wa Azam Comlex ulioko Chamazi.
Azam FC inakuwa timu ya tatu kwenye ligi hiyo ukiachana na Simba na Mtibwa Sugar, kufanikiwa kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo msimu huu baada ya kufikisha jumla ya pointi saba.
Bao pekee la Azam FC limefungwa na mshambuliaji Mbaraka Yusuph dakika ya 43 akimalizia pasi ya safi aliyopenyezewa na Yahya Zayd, aliyewahadaa mabeki wa Kagera Sugar kabla ya kumsetia Yusuph.
Hilo ni bao la kwanza la mashindano la Yusuph tokea ajiunge na Azam FC, akiifunga timu yake ya zamani aliyoichezea msimu uliopita kabla ya kutua kwa matajiri hao wa viunga vya Azam Complex msimu huu.
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi walifanikiwa kucheza vema kwenye mchezo huo hasa kipindi cha kwanza, wakionyesha kandanda la kasi huku Yusuph na Zayd wakionekana kuwa kivutio baada ya kuipa wakati mgumu safu ya ulinzi ya Kagera Sugar.
Kwa ushindi huo, hivi sasa Azam FC imefanikiwa kuandika rekodi ya kipekee baada ya kucheza mechi tatu za mwanzo za ligi bila kuruhusu wavu wake kuguswa (cleensheet) ikiwa imefunga mabao mawili tu.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kwa siku mbili leo na Jumapili kabla ya kurejea mazoezi Jumatatu asubuhi kujiandaa na mtanange ujao dhidi ya Lipuli utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi ijayo Septemba 23 saa 1.00 usiku.
Kikosi cha Azam FC:
Razak Abalora, Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris, Himid Mao (C), Yahya Zayd/Braison Raphael dk 77, Frank Domayo/Stephan Kingue dk 87, Yahaya Mohammed/Idd Kipagwile dk 37, Salum Abubakar, Mbaraka Yusuph.
Post a Comment