CHIRWA AIPELEKA KILELENI YANGA
Timu ya soka ya Yanga ya jijini Dar es salaam imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 mbele ya wachimba madini wa mkoani Shinyanga Mwadui FC katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Yanga imefanikiwa kuibuka na ushindi huo kupitia kwa mshambuliaji wake Obrey Chirwa aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Haruna Niyonzima ambapo mabao yake mawili yameiweka kileleni timu yake katika msimamo wa ligi kuu ya Tanzania bara.
Mwadui walionekana dhahiri kuibana Yanga katika kipindi cha kwanza kwani walijalibu kufanya mipango ambayo iliwapa wakati mgumu kina Haruna Niyonzima,Amisi Tambwe pamoja na Saimon Msuva ambao waliongoza safu ya ushambuliaji kwa upande wa Yanga.
Timu hizo zimaliza kipindi cha kwanza pasipo kufungana,ambapo waliporejea katika kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko ya wachezaji ambapo mabadiliko hayo yaliwanufaisha zaidi Yanga kwani walifanikiwa kupata mabao 2 katika kipindi hicho.
Baada ya dakika tisini za mchezo huo kukamilika kwa wenyeji kuzoa alama tatu muhimu na kuwaweka kileleni kwenye msimamon wa ligi kuu ya Tanzania bara,kocha msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi amewapongeza wachezaji wake kwa kucheza kwa juhudi kubwa na kufanikiwa kuibuka na ushindi.
"Mchezo wa leo ulikuwa mgumu kwa upande wetu hasa kipindi cha kwanza kwani wapinzani wetu dhahiri walionekana kuziba mianya ili tusifunge lakini kipindi cha pili tumefanya marekebisho ambayo yametupa faida tukashinda"alisema Mwambusi.
Kwa upande wake kocha msaidizi wa timu ya Mwadui, Khalid Adam amesema kwamba makosa yaliyofanywa na wachezaji wake ndio yamewagharimu kufungwa katika mchezo wa leo dhidi ya mabingwa watetezi wa kombe hilo Yanga.
Amesema kwamba vijana wake walicheza kwa umakini zaidi hasa kipindi cha kwanza lakini makosa ya kiuchezaji ndio yamewafanya wapinzani wao kuchomoza na ushindi.
Post a Comment