TFF YAZINDUA KAMPENI ZA KUFUZU OLIMPIKI

Mkurugenzi wa michezo,Yusuph Omari,Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF,Jamali Malinzi kwa kushirikiana na makamu wa Rais wa kamati ya Olimpiki Tanzania {TOC},Henry Tandau hii leo wamezindua rasmi kampeni maalumu za kuifanikisha Tanzania kushiriki michuano ijayo ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo,Japan mwaka wa 2020.

Akiongea mbele ya waandishi wa Habari leo hii wakati wa uzinduzi huo,Mkurugenzi wa michezo Yusuph Omari amesema kwamba Tanzania haiwezi kufanikiwa kwa mchezo wowote bila ya kuwepo kwa programu ya vijana.

"Katika kuhakikisha azma hiyo inafanikiwa ni vyema watanzania kwa pamoja tukaelekeza nguvu zetu kwenye mpango wa kukuza vijana kwani kufanya hivyo kutaleta tija kwa nchi hasa kwenye maendeleo ya michezo"alisema Omari.

Alisema kwamba kwa kulitambua swala hilo Serikali itakuwa bega kwa bega na TFF ili kuhakisha wanafanikiwa kushiriki Olimpiki ya mwaka 2020 kwa kupeleka timu mbalimbali ikiwemo ya mpira wa miguu.

Nae Rais wa TFF,Jamali Malinzi amesema kwamba mbali na kushiriki michuano ya Olimpiki lakini lengo kuu ambalo linaendelea kufanywa na shirikisho hilo ni kuona Tanzania inafanikiwa kucheza fainali za kombe la dunia zitakazofanyika mwaka wa 2026.

Malinzi amesema kwamba kwa sasa shirikisho hilo linaendelea kuboresha timu za vijana ambao ndio watakuwa msada kwa timu za Taifa katika kampeni hizo za kufuzu kwa mashindano hayo.

Alisema kuwa anaamini mpango huo ambao unafanywa na TFF juu ya timu za vijana wakiwemo Serengeti Boys ambao kwa mujibu wa taarifa yake amedai kuwa hadi siku ya alhamisi watatambua juu ya vijana hao kucheza fainali za vijana wa Afrika utakuwa na tija kubwa ya kuleta maendeleo ya mpira wa miguu hapa nchini.

Alisema kwamba kuna mpango maalumu ambao wanataraji kuuzindua wakati wowote kuanzia sasa kwa ajili ya kuendeleza mpira wa vijana, ambapo mpango huo utakuwa na mfuko maalumu na Ofisi zake zitakuwa maeneo ya Mikocheni ukiwa na lengo la kukusanya rasilimali kwa ajili ya kuwekeza kwenye soka la vijana.

"Nawaasa watanzania kuwa watulivu kwa wakati huu hasa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa TFF,kwani kutaibuka makundi ambayo yatakuwa na nia ovu ya kuharibu mipango yenye maendeleo katika mpira wa miguu"alisema Malinzi.

No comments