TWIGA STARS KUJIULIZA TENA KWA CAMEROON JUMAPILI
Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu Wanawake ‘Twiga Stars’ jana Novemba 10, 2016 ilipoteza kwa taabu mchezo wake wa kwanza wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya wenyeji Cameroon ambayo ilipata mtihani mzito kwa Watanzania kwa dakika zote kabla ya kuibuka kwa ushindi wa mabao 2-0.
Cameroon ambayo ilijipanga kushinda mabao mengi, ilitolewa jasho na hivyo kuomba mchezo mwingine ambao sasa utafanyika Jumapili Novemba 13, mwaka huu jijini Yaounde na Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Sebastian Nkoma amesema: “Nimeona upungufu katika mchezo wa jana, nafanyia kazi.”
Bao la kwanza katika mchezo wa jana lilifungwa na Mshambuliaji Ngoya Ajara wa Klabu ya Sundsvalls ya Sweden ambaye pia ndiye Mchezaji Bora wa mwaka 2016 nchini Cameroon wakati bao la pili lilifungwa na Kiungo wa Klabu ya Aurillac ya Ufaransa Ngono Mani Michelle katika dakika ya 71.
Twiga Stars wao wamealikwa na Waandaaji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake 2016 – Cameroon ambao wameamua kuipa heshima Tanzania na kuona kuwa timu hiyo ina ubora wa na kwamba inafaa kuipimana ubavu kabla ya kuanza kwa fainali hizo Novemba 19, mwaka huu.
Twiga Stars ambayo sehemu kubwa ya kikosi hicho kinaundwa na wachezaji wa timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania Bara yaani Kilimanjaro Queens ina rekodi nzuri ya kuwa kinara wa viwango vya ubora kwa nchi za Afrika Mashariki na kati lakini zaidi ni mabingwa wapya wa ukanda huo – ubingwa uliopatikana Septemba, mwaka huu huko Uganda.
Rekodi hizo zimesukuma Shirikisho la Mpira wa Miguu la Cameroon (FECAFOOT) – nyumbani kwa Rais wa CAF, Issa Hayatou kuikubali Twiga Stars na hivyo kuomba kucheza nayo mwishoni mwa wiki hii. Tayari Twiga Stars imeanza maandalizi ya kutosha chini ya Makocha Sebastian Nkoma na Wasaidizi wake Edna Lema na El Uterry Mohrery.
Kikosi cha Twiga Stars wamo makipa, Fatma Omari na Najiat Abbas; mabeki ni Wema Richard, Sophia Mwasikili, Anastasia Katunzi, Maimuna Hamisi, Fatuma Issa, Happiness Mwaipaja na Mary Masatu wakati viungo ni Donisia Minja, Stumai Abdallah, Amina Ally, Anna Mwaisura na Fadila Kigarawa ilhali washambuliaji ni Fatuma Swalehe, Asha Rashid na Mwanahamisi Omari.
Wakati huo huo, taarifa kutoka zinasema timu ya taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imefungwa bao 1-0 na Seongnam katika mchezo wa kwanza wa kuwania Kombe la Korea Kusini katika michuano iliyoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Korea Kusini. Mchezo huo ulifanyika jijini Seoul, Korea Kusini na goli moja lililofungwa kipindi cha kwanza, vijana wetu wameonesha uwezo mkubwa sana.
Kikosi kilicho anza ni Ramadhani Kabwili (1), Kibwana Ally (12), Nickson Kibabage (3), Ally Msengi (14), Dickson Job (5), Ally Ng'azi (2), Shaban Zubeir (13), Asad Juma (10), Mohamed Rshid (11), Nashon Kelvin (7), na Muhsin Makame (19). Kipindi cha pili benchi la Ufundi lilifanya mabadiliko aliingia Cyprian Mtesi (8) Kuchukua nafasi ya Muhsin Mkame (2) na Errick Nkosi (4) kuchukua nafasi ya Ally Ng'anzi (2).
Post a Comment