LIGI YA VIJANA U20, UZINDUZI BUKOBA NOV. 15
Ligi ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 za klabu zote za Ligi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kuanza Novemba 15, 2016 kwa mchezo maalumu wa ufunguzi utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linachukua nafasi hii kuzikumbusha klabu kuwa zina taarifa kuhusu kuwako kwa ligi hiyo ya U20 na kwamba mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa ni Novemba 3, mwaka huu katika barua maalumu kwa kila klabu yenye Kumb. Na. TPLB/CEO/2016/036.
Tayari klabu hizo zimepewa shilingi milioni 10 (Sh 10,000,000) kutokana na udhamini wa Benki ya DTB kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo. Pia kila klabu itapewa shilingi milioni 10 (Sh 10,000,000) nyingine kutokana na udhamini wa matangazo ya ligi ya U20 wa Azam Tv.
Kwa udhamini huo kila klabu itajigharimia usafiri wa kwenda na kurudi kituoni, malazi, na chakula kwa kipindi chote cha mashindano. Vituo vilivyopangwa ni Dar es Salaan ambako kuna timu za JKT Ruvu, Simba, Ruvu Shooting, Ndanda, Majimaji ya Songea, Mtibwa, Mbeya City na Tanzania Prisons.
Kituo kingine ni Bukoba mkoani Kagera ambako kuna timu za Azam, African Lyon, Mbao FC, Toto Africans, Mwadui ya Shinyanga kama ilivyo Stand United, Kagera Sugar na Young Africans ambazo zitafungua dimba hiyo Novemba 15 kwa mchezo pekee.
Tunazikumbusha klabu kuzingatia Kanuni ya 42 (27) ya Ligi Kuu ya Vodacom inayosema: “Klabu ambayo haikupeleka uwanjani timu ya U20, mechi ya kwanza itapigwa faini ya Sh 2,000,000 na kunyang’anywa na kupoteza mchezo, mechi ya pili itapigwa faini ya Sh 2,000,000 na kunyang’anywa pointi tatu katika Ligi ya Wakubwa (Ligi Kuu) na Ligi ya Wadogo (u20).
Pia tunazikumbusha klabu kuwa kwa mujibu wa Kanuni, wachezaji saba (7) kutoka U17 wanaruhusiwa kuchezea timu ya U20. Ruhusa hiyo ni kwa wachezaji wa U17 waliosajiliwa, kwa maana kuwa katika ligi zote wachezaji wanatambuliwa kwa kutumia leseni.
Post a Comment