GEORGE LWANDAMINA MBIONI KUJIUNGA NA KLABU YA YANGA

Uongozi wa mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania bara timu ya soka ya Yanga umesema kwamba kujiuzulu kwa kocha wa timu ya Zesco ya Zambia George Lwandamina hakuna mahusiano yeyote na yeye kujiunga na klabu ya Yanga.

Kaimu katibu mkuu wa Yanga Baraka Deusdedit amesema kwamba kwa upande wake kama mtendaji mkuu wa klabu hana hizo taarifa ispokuwa amedai kuwa kama kutakuwa na makubaliano yeyote kwa pande zote basi klabu itatoa taarifa rasmi kwa wanachama wao.

Hata hivyo Baraka amewataka wanachama wa klabu hiyo kuendelea kuwa wamoja na timu yao kwani ligi bado ni ngumu na kama uongozi utafanya mabadiliko yoyote basi ni kwa ajili ya manufaa ya klabu.

Mapema leo hii uongozi wa timu ya Zesco ya Zambia umetoa taarifa ya kupokea barua ya kocha Lwandamina ya kujiuzulu ambapo uongozi huo nao umeridhia jambo hilo.

No comments