WAZIRI MKUU AAGIZA BMT ICHUNGUZWE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe alifanyie mapitio Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na iwapo hatoridhika na utendaji wake alivunje.

“Ninamuagiza Waziri mwenye dhamana kufanya mapitio na kutathmnini upya utendaji kazi wa Baraza la Michezo Tanzania juu ya usimamizi wake wa  michezo nchini na kama hataridhika, anayo mamlaka ya kulivunja Baraza hilo.”  

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Julai 5, 2017) katika hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge mjini Dodoma.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano haitafumbia macho usimamizi mbovu na utawala wa michezo usiojali maslahi ya Taifa. “Serikali imeazimia kuimarisha utendaji kwa vyombo vya michezo nchini ili kila mwenye dhamana awajibike ipasavyo.”


No comments