SINGIDA UNITED YAMUADHIBU KAMBALE

Na,Said Ally
Klabu ya Singida United inayoshiriki ligi kuu ya Tanzania bara imemsimamisha mchezaji wake Kambale Salita Gentil,kufanya kazi ndani ya klabu hiyo hadi hapo uongozi utakapoamua vinginevyo.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo Festo Richard Sanga amesema kwamba uongozi umechukua jukumu hilo la kumsimamisha Kambale baada ya mchezaji huyo kuzawadiwa kadi nyekundu katika mchezo wao wa jana wa kombe la FA dhidi ya Green Warriors.

Sanga alisema kwamba mchezaji huyo ameigharimu timu katika mechi hiyo baada kufanya tukio baya lisilo la uwanamichezo ambalo lilipekea mchezaji kupewa kadi nyekundu na kusababisha timu kucheza pungufu kwenye pambano hilo lililomalizika kwa Singida United kutinga katika hatua ya 16 bora kwa changamoto ya mikwaju ya penati 4-3.

Alisema kwamba mbali na mchezo huo wa FA pia katika Mechi ya Singida United na Tanzania Prison  Kambale akitambua klabu inahitaji ushindi, alitumia zaidi ya dakika tano  za mchezo kugombana na mchezaji wa timu pinzani tena bila mpira, na hata kaptain wa timu na mwamuzi walipoingilia kati aliendelea na mzozo na kupewa onyo kwa kadi ya njano, uongozi ulituma benchi la ufundi kuzungumza na mchezaji kuhusu kitendo hicho lakini inaonekana kama anajenga mazoea juu ya kitendo hicho.

Kambale raia wa Congo alisajiliwa na Singida United katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo kwa ajili ya kukiongeza nguvu kikosi cha Singida United ambacho kinapigania nafasi ya kutwaa taji la ligi kuu ya Tanzania bara na michuano ya kombe la FA.

No comments