IDD CHECHE KUIONGOZA AZAM FC

Uongozi wa klabu ya Azam FC leo hii umetangaza rasmi kuachana na makocha wake kutoka nchini Hispania kutokana na kutoridhishwa na kiwango cha ufundishaji wao katika timu hiyo.

Jopo hilo la makocha linaundwa na Kocha Mkuu Zeben Hernandez, Msaidizi wake, Yeray Romero, Kocha wa Makipa Jose Garcia, Kocha wa Viungo, Pablo Borges na Mtaalamu wa tiba za Viungo, Sergio Perez.

Uamuzi huo umefikiwa na Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo jana, na umetokana na mwenendo mbaya wa Azam FC kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), ambayo imefikia raundi ya pili hivi sasa.

Azam FC inawatakia kila la kheri na mafanikio mema makocha hao huko waendako na inawashukuru kwa mchango wao wote walioutoa kwenye timu kwa kipindi chote walichokaa, ikiwemo kuwapa taji la kwanza la Ngao ya Jamii mwaka huu kwa kuifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2.

Wakati huu ambapo uongozi wa Azam FC upo katika mchakato wa kusaka kocha mpya, kikosi hicho kitakuwa chini ya makocha wa timu ya vijana ya timu hiyo, Idd Cheche na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar, ambao walianza kazi jana jioni kukiandaa kikosi kuelekea mchezo wa leo dhidi ya Tanzania Prisons.

No comments